Alhamisi, 12 Juni 2014

TAMATHALI ZA SEMI KATIKA FASIHI Tamathali za semi ni maneno, nahau au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii ili kutia nguvu katika maana, mitindo na hata sauti katika maandishi ama kusema. Wakati mwingine hutumiwa kama njia ya kuipamba kazi ya fasihi na kuongeza utamu wa lugha (Senkoro, 1984:13). Hii ina maana kwamba ili msomaji wa kazi yoyote ya fasihi apate ujumbe hana budi kufikiri kwa kina. Pia tamathali za semi ni fungu la maneno lililogeuzwa maana yake kamili ili kiuwakilisha maana nyingine (Msokile, 1992:210). Akiwa na maana kuwa katika tamathali zipo maana na matumizi mengine ya kisanii ambayo msanii anapaswa kuyatumia ili aweze kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira. Tamathali za semi ni viwakilisho au vifananisho vya dhana fulani kwa dhana nyingine tofauti zinazo fanana. Huu ni usemi unaobadilisha maana dhahiri au za kawaida za maneno ili kuleta maana maalumu ya fasihi iliyokususudiwa na msanii. (Mwamanda, 2008:42). Kwa ujumla tamathali za semi ni maneno au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii au waandishi wa kazi za fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata katika sauti za kusema au maandishi. Hutumika katika fasihi kwa lengo la kuipamba kazi ya fasihi na kuongeza utamu katika lugha iliyotumika katika kazi husika. Tamathali hizi huweza kugawanyika katika vipengele tofautitofauti kama vile tamathali za mlinganisho, tamathali za mafumbo, tamathali za msisitizo pamoja na tamathali nyingine za semi. Vipengele vya tamathali za semi ni muhimu sana katika kuunda au kutoa msisitizo wa maana pamoja na kuunda maana mpya katika kazi za fasihi, vipengele hivyo huweza kufafanuliwa na kuweza kutumika katika kazi za kifasihi kwa namna tofautitofauti kama ifuatavyo: Tashibiha au Mshabaha ni aina mojawapo ya tamathali za semi inayofanya kazi ya kulinganisha vitu viwili visivyo na hadhi sawa kwa kutumia viunganishi kama; mithili ya, mfano wa, sawa na kama vile. Mara nyingi aina hii ya tamathali za semi huweza kufanya kazi endapo tu pana vitu viwili vinavyolinganishwa, wakati kimoja hutumiwa katika kukirejelea na kuelezea kingine na aghalabu kimoja kati ya vitu hivyo huwa kinaeleweka na hivyo hutumiwa ili kuangazia hicho kingine. Mfano katika tamthilia ya “Ngoma ya Ng’wana malundi” (Mbogo, 2008) anasema: “Vizuu wanakula kwa kupokezana kama nguruwe au vichaa” (Uk. 18). “Uso uliparama kama jiwe la kiama” (Uk. 8). Pia katika riwaya ya “Janga sugu la wazawa” ( Ruhumbika, 2001:88) anasema: “Basi siku hiyo hiyo Bugonoka alitambua hali hiyo mpya ya mama yake nayo pia ni sehemu ya janga lake na watu wake hapa duniani, sawa kabisa na kifo cha baba yake............” Kwa kutumia tamathali hii ya semi wasanii wameshushughulikia mambo makuu matatu ambayo ni Kizungumzwa, Kifananishi na Kiungo. Kizungumzwa ni kitu halisi ambacho huzungumzwa na kitu kinachofananishwa kwa fumbo, kifananishi kipo katika mawazo na huzingatia maana dhahania na kiungo ni sifa zipatikanazo katika kitu kinachozungumzwa. Kazi yake kuu ni kuhusisha vitu vyote viwili katika kuunda maana kama inavyoonekana katika mifano hapo juu. Takriri ni aina nyingine ya tamathali za semi ambayo yenyewe huhusika na urudiajirudiaji wa maneno, silabi au sauti zinazolingana katika kazi ya sanaa. Mwandishi huamua kwa makusudi kurudirudia maneno au vipengele hivyo kwa lengo maalumu kwa kusisitiza jambo ama kuleta mkazo wa jambo linaloelezwa (Msokile, 1992:61). Kwa mfano, katika riwaya ya “Rosa Mistika ” (Kezilahabi, 1971:67) takriri inaonekana kama ifuatavyo: “Rosa, Rosa, Rosa, mtoto wangu, mimi ninakufa. Njoo karibu nikuguse, njoo nikupe baraka yangu ya mwisho.” Pia katika tamthilia ya “Nguzo Mama” (Muhando, 2007:13), takriri inajitokeza kwa kutumia walevi

Maoni 3 :

  1. N vyem kuelimisha fasihi ni kiipotosh jamii

    JibuFuta
  2. N vyem kuelimisha fasihi ni kiipotosh jamii

    JibuFuta
  3. N vyem kuelimisha fasihi ni kiipotosh jamii

    JibuFuta